Seventh-day Adventist® Church

Northern Tanzania Union Conference

Menu
MATAMKO YANAYOTAMBULISHA KANISA NA UTENDAJI WAKE JINSI ULIVYO
(Tafsiri imefanywa na Mch E. Kasika, Mratibu wa Mpangokazi na Utume wa Kanisa, Nov. 2014)

I.      UTANGULIZI:  KUIELEWA CHANGAMOTO INAYOLIKABILI KANISA
    1. Kanisa la Kristo linaelezwa katika Agano Jipya kuwa ni moja, alilolianzisha yeye, na akihudumu kama kichwa cha Kanisa. (Mathayo 16:18,19; Kolosai 1:16-18; Efeso 5:22,23).
    2. Kristo ameliwekea Kanisa misingi inayoongoza utume wake na na jinsi ya kutenda kazi ili kutimiza utume wake, msingi mkuu ukiwa ni kuongozwa na kweli yake, (1Timotheo 3:15,16).
    3. Mwenendo wa kanisa haukuachiwa mtizamo binafsi au wa kikundi kidogo cha waumini, bali umetolewa na Kristo mwenyewe, unaotakiwa kuzingatiwa ili waumini wastahili kuitwa wanafunzi wake. (Yohana 15:7,8,16; Kolosai 1:10-12; 1Yohana 2:6).
    4. Miongoni mwa maombi mengi waumini watakiwayo kuomba ili wastahili kutenda itakiwavyo kanisani, ni maombi ya kujazwa maarifa ya  mapenzi ya Mungu katika hekima yote na ufahamu wa rohoni, (Kolosai 1:9), ili wafaulu wafaulu kuenenda kama ulivyo wajibu wao kwa Bwana, wakimpendeza kabisa,; na wakizaa matunda kwa kila kazi njema, na kuzidi katika maarifa ya Mungu; wakiwezeshwa kwa uwezo, kwa kadri ya nguvu ya utukufu wake Mungu, (Kolosai 1:10).
    5. Kristo aliliombea kanisa lake ili lidhihirishe utendaji wenye umoja katika Mungu mmoja; umoja wa imani, umoja wa mafundisho na umoja wa huduma,(Yoh 17:20-26; Efe 4:1-7).
    6. Kama matokeo ya athari za manabii  na waalimu wa uongo wanaojipenyeza ndani ya Kanisa kila kizazi, kanisa hujikuta likiyumbishwa na mafundisho ya uongo kiasi cha kulifanya litoke katika kweli ya Kristo, na kuendekeza mitizamo ya uelewa binafsi ya waumini wachache, kwa faida binafsi, (2Petro 2:1-3; Galat 2:4,5; Yuda 1:3,4). Kanisa linalazimika kila wakati kukabiliana na waalimu na manabii wa uongo wanaotaka watambulike kama ndugu katika imani.
    7. Kadri madhehebu yanavyozidi kuibuka ndani ya kanisa la Kristo, kila moja likidai kuwa na haki na kweli kuzidi jingine, Kanisa la Waadventista Wasabato linalazimika kutoa matamko yanayolifanya litambulike ni kanisa gani, kwa nini lipo na linavyoendesha utume wake ili utofauti wake na madhehebu mengine uwe bayana.
 
  1. II.     MATAMKO YA KANISA YANAYOELEKEZA UTENDAJI ULIVYO
Kanisa la Waadventista Wasabato lina matamko kadhaa yanayoelekeza utendaji wake jinsi ulivyo. Matamko hayo ni sehemu ya sera za Kanisa ambayo hutakiwa kueleweka vizuri kwa kila muumini na kwa watu wengine wanaotaka kujua habari za msingi za Kanisa hili. Matamako ya lazima kueleweka ni yafuatayo:
  1. Tamko la Utume wa Kanisa la Waadventista Wasabato, (The Mission Statement of the Seventh – day Adventist Church). Kusudi la Tamko hili ni kulitambulisha Kanisa kwa wasiolijua, likieleza Utume  wa Kanisa, Utambulisho wa Kanisa na Utekelezaji wa utume  wa Kanisa ulivyo na sababu ya kutekeleza namna hiyo, (Njozi ya Kanisa).
  2. Tamko la Kujitoa Kikamilifu kwa Mungu, (A statement of Total Commitment to God). Linamwelekeza muumini ajue anavyotegemewa adhihirishe kujitoa kwake kwa Mungu, katika kila fani ya utendaji wa kanisa.
  3. Mwongozo wa Kanisa, (Zamani: Kanuni ya Kanisa)- (Seventh –day Adventist Church Manual).
Hili sio tamko moja bali ni kitabu kinachotumiwa na Kanisa mahalia, kinachoelekeza kanuni zia kuzingatia katika utendaji wa kila siku kanisani. Ndani ya Mwongozo huu kunaelezwa: Kanuni mbalimbali za kiutendaji;  Taratibu za kufuatwa; Misingi ya Imani kimafundisho;  majukumu na uwajibikaji  wa watendakazi katika nyadhifa mbalimbali.
Katika kitini hiki nimeambatanisha Matamko mawili tu A,na B juu ili yafundishwe na kueleweka  katika ngazi ya Kanisa Mahalia, kwa imani kuwa Mwongozo wa Kanisa/ Kanuni ya Kanisa unaeleweka vizuri.
 
 
  1. A.    TAMKO LA UTUME WA KANISA LA WAADVENTISTA WASABATO, (Sahihisho la 2014).
 
UTUME WETU (OUR MISSION) – Utume wa Kanisa la Waadventista Wasabato  ni kuwaita watu wote wawe wanafunzi  wa Yesu, kutangaza Injili ya milele katika muktadha wa Ujumbe wa Malaika watatu wa Ufunuo 14:6-12, na kuandaa ulimwengu marejeo ya Kristo yaliyo karibu.
UTEKELEZAJI WA UTUME WETU (OUR METHOD) – Kwa kuongozwa na Biblia na Roho Mtakatifu, Waadventista Wasabato hutekeleza utume huu kupitia maisha yanayoakisi alivyoishi Kristo, katika kuwasiliana, kufanya wanafunzi, kufundisha, kuponya, na kuhudumia.
NJOZI YA UTUME WETU (OUR VISION) – Kwa kupatana na mafunuo ya Biblia, Waadventista  Wasabato tunauona utume wetu ukifikia kilele katika mpango wa Mungu wa urejeshwaji wa viumbe vyake katika ukamilifu wa mapenzi yake na haki yake.
TAMKO LA UTAMBULISHO NA UTEKELEZAJI WA UTUME WETU
UTAMBULISHO WETU, (Our identity)
Kanisa la Waadventista Wasabato linajielewa kuwa ni Kanisa la masalio la unabii wa Biblia wa siku za mwisho (the remnant Church of end-time Bible prophecy). Washiriki wa Kanisa hili, mmoja mmoja au kwa pamoja, huelewa  jukumu lao maalumu kama mabalozi wa ufalme wa Mungu,  na wajumbe wa marejeo ya Yesu Kristo yaliyo karibu. Waadventista Wasabato wamejiandikisha kama jeshi la wafanyakazi pamoja na Mungu katika utume wa kuurejesha ulimwengu kutoka katika nguvu na uwepo wa uovu, kama sehemu ya Pambano Kuu baina ya Kristo na Shetani.
 
Kwa hiyo, kila hali ya maisha ya mshiriki wa Kanisa huathiriwa na kusadiki na kuamini kuwa tunaishi katika siku za mwisho za unabii wa Biblia na kwamba kurudi kwa Yesdu Kristo kuko karibu sana.Waadventista Wasabato wameitwa na Mungu kuishi katika ulimwengu huu.Kila tendo la maisha ya Mkristo hufanyika “katika jina la Yesu” na kutangaza ufalme wake, (and to advance His kingdom).
 
UTEKELEZAJI WA UTUME WETU (Implementation of our Mission)
Waadventista Wasabato hukiri kwa dhati kuwa Maandiko Matakatifu, Biblia, ni ufunuo wa mapenzi ya Mungu usio na makosa, hukubali mamlaka yake(Biblia)  katika maisha ya Kanisa na ya kila muumini, na kwamba ndicho kipimo cha imani na mafundisho.  Waadventista Wasabato huamini kwamba Roho Mtakatifu ndiye uwezo unaobadili maisha yetu mwenye kuwapatia watu vipaji vya kutangaza ufalme wa Mungu katika ulimwengu huu.
 
Wakiwa wameitwa na Mungu, na kuongozwa na Biblia, kwa kuwezeshwa na Roho Mtakatifu, Waadventista Wasabato, kokote tunakoishi ulimwenguni, kwa moyo wa kupenda kufanya kazi hujitoa kufanya yafuatayo:

Kuishi kama alivyoishi Kristo – Kadri tunavyoishi tutaonesha kuwa Kristo ndiye Bwana wetu kimaadili, kiutamaduni na kimwenendo katika jamii, kwa kuongozwa na mafundisho yake muda wote na tukiiga mfano wake.

Kuwasiliana kama alivyowasiliana Kristo- Tukielewa kuwa sote tumeitwa  tushuhudie kwa nguvu, tunashiriki  kwa njia ya mazungumzo binafsi, mahubiri, uchapishaji na stadi mbalimbali,  ujumbe wa Biblia juu ya Mungu, tumaini tulilonalo na wokovu uliotolewa naye kupitia maisha, utume, kifo, ufufuo na huduma ya ukuhani wa Yesu Kristo.

Kufanya wanafunzi kama alivyofanya Kristo- Kwa kuthibitisha ukuaji wa kiroho ulio endelevu kwa maendeleo ya waumini, tunatoa malezi kwa waumini wapya, tukiwafunza kuishi maisha ya haki na kuwaelekeza kushuhudia kwa mguso wenye nguvu na kuwatia shime kuonyesha mwitikio wa utii kwa mapenzi ya Mungu.

Kufundisha kama alivyofundisha Kristo- Tukikiri kwamba maendeleo ya mwili na tabia ni vya muhimu katika mpango wa Mungu wa Ukombozi, tunahimiza ukuaji katika kumwelewa Mungu na jinsi ya kuhusiana na Yeye, na Neno lake, pamoja na vitu vyote alivyoviumba.

Kuponya kama alivyonya Kristo- – Kwa kuzithibitisha kanuni za Biblia za kuwa na utu wote mkamilifu (Well-being of the whole person), tunafanya utunzaji wa afya zetu na uponyaji wa wagonjwa kuwa kipaumbele chetu.  Kwa kuwahudumia maskini na wanaoteseka, tunashirikiana na Muumba katika kazi yake ya urejeshwaji kwa njia ya matendo ya huruma.

Kutumika kama alivyotumika Kristo – Kwa kufuata kielelezo cha Yesu tutajitoa kuwa na utumishi wenye unyenyekevu, tukiwahudumia watu na jamii za watu walioathiriwa zaidi na umasikini, misiba, wasio na matumaini na wagonjwa.
© 2018 Northern Tanzania Union Conference